Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo katika eneo la Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara sasa imefikia 65, wale waliojeruhiwa ikifikia 116 kulingana na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Rais Samia Suluhu ameagiza Waziri Mkuu Kassim Majaaliwa kuhakikisha waliojeruhiwa wanatibiwa kwa gharama ya serikali.
Taarifa kutoka Ikulu imesema Rais Samia ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao.
Rais Samia ambaye amekuwepo Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ameamua kufupisha safari hiyo na kurejea nchini haraka iwezekanavyo ili kushughulikia kwa karibu janga hilo.
Waliojeruhiwa wamekuwa wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa hali zao zinapokuwa zimeimarika na wengine wamekuwa wakipelekwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu na kuondoka.
Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jumapili imesababisha mafuriko ya tope zito katika eneo hilo.
Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema eneo kubwa lililoathirika na mafuriko hayo ni kata ya Gendabi katikati ya mji wa Katesh.
Bi. Sendiga ameiambia BBC kwamba Serikali imeongeza juhudi za kufukua vifusi kuondoa miili katika tope zito.
''Kitu kama hiki kinapotokea cha ghafla watu hukimbia kimbia, mwingine anakwambia simuoni mtoto wangu, hapa hajaonekana, kwahiyo tulichofanya kwanza tumejaribu kupita kule kwenye eneo ambalo changamoto ilianzia na tumewaambia wapite hospitali kuangalia miili iliyo hospitalini na wagonjwa waliolazwa huko'' Alisema.
Kikosi cha kupambana na maafa chini ya Ofisi ya Waziri mkuu kimetumwa Katesh kufanya shughuli mbalimbali za uokoaji ambapo tayari kambi tatu zimeandaliwa kwa ajili ya kuwapatia hifadhi watu waliokosa kabisa mahali pa kuishi.
‘’Kikosi maalumu cha jeshi kimetumwa usiku kusaidia kuopoa miili iliyokwama katika tope na kurejesha miundo mbinu katika hali yake ya kawaida’’
Aidha Wananchi wamesisitizwa kuhama katika maeneo hatarishi ikiwemo chini ya milima na katika maeneo ya mabonde.
Comments